board and brain

Kama ni mfuatiliaji wa  mambo yanayohusu teknolojia ni rahisi kuwa umeshakutana na maneno Artificial Intelligence au AI kwani kwenye ulimwengu wa technolojia kwa sasa Artificial Intelligence ni moja kati ya mambo yanayosikika sana.

Artificial Intelligence ni nini?

Artificial Intelligence ni matumizi teknolojia yanayowezesha kompyuta au mashine kufanya mambo ambayo kwa kawaida huhitaji kutumia uwezo wa kiakili kama binadamu kwa mfano kutambua vitu, watu, lugha, sauti, kufanya maamuzi, kutabiri, kutafsiri, kujifunza, ... nakadhalika.

Unaposikia Artificial Intelligence unaweza kuadhani hii inahusika tu maroboti na teknolojia za hali ya juu kupindukia, ambazo hujawahi na hutawahi kuzitumia katika maisha yako. Japo Artificial Intelligence pia hutumika kwenye maroboti na teknolojia nyingine kubwa za hali ya juu, Artificial Intelligence pia inatumika katika teknolojia nyingi za kawaida zinatumiwa na watu wengi katika maisha ya kila siku.

Mifano ya matumizi ya Artificial Intelligence

Unaweza kujiuliza... Je umewahi kutumia vitu vinavyotumia Artificial Intelligence?

Kama umewahi kutumia Google, Facebook, Twitter, Gmail, Yahoo, Instagram, YouTube, Uber, Snapchat au kamera ya smartphone yako katika siku za hivi karibuni kuna uwezekano wa zaidi ya asilimia 99 kuwa umeshawahi kutumia au kunufaika na Artificial Intelligence.

Artificial Intelligence inaweza kutumika kwa namna nyingi sana. Mifano michache ya vitu vinavyotumia Artificial Intelligence katika teknolojia zilizozoeleka katika maisha ya kila siku inaweza kusaidia kuelezea Artificial Intelligence ni nini na inaweza kutumikaje.

Gmail

Barua pepe zako unazopata kwa kupitia Gmail huwa zinagawanywa kwa makundi mbali mbali kwa mfano primary (za msingi), spam (za kupuuzia au za kitapeli), social (mitandao ya kijamii), promotions (matangazo), nakadhalika. Kwenye hili badala ya wewe kufanya kazi ya kutambua na kupangilia barua pepe katika makundi, Artificial Intelligence inayotumiwa kwenye mfumo wa Gmail inakusaidia kufanya kazi hiyo kiautomatiki.

Mfano mwingine ni pale unapoandika barua pepe ya Kiingereza, unaweza ukaona Gmail inakupendekezea maneno au sentensi ya kuandika kwa usahihi kulingana na muktadha husika. Haya pia ni matokeo ya matumizi ya Artificial Intelligence.

Youtube

Mfano unapoangalia video ya wimbo kwenye YouTube mara nyingi huwa unapendekezewa video nyingine za kuangalia. Mara nyingi video hizo huwa ni nyimbo au video  zinazoendana sana na wimbo unaouangalia kwa wakati huo. Hapo kinachotokea ni kwamba mfumo wa  YouTube hutumia Artificial Intelligence ili kutambua video nyingine zinazofanana na video husika.

Kamera za smartphone

Kwenye kamera nyingi za smartphone za siku hizi napojipiga selfie kwenye skrini huwa kinatokea kiboksi kinatokea kuuzunguka uso wako, na kila unapousogeza uso wako kiboksi hicho huwa kinasogea pia kuufuata na hii inakusaidia kujiselfisha vizuri zaidi. Hapa Artificial Intelligence inatumika kutambua uwepo wa uso wa binadamu kwenye picha.

Google search

Ukiamua kutafuta kwenye Google kwa mfano "What is AI". Google hutumia Artificial Intelligence kutambua kuwa unauliza swali na kujaribu kutambua jibu la moja kwa moja kuhusu Artificial Intelligence ni nini.

...

Hii ni mifano michache tu kati ya mifano mingi sana ya matumizi ya Artificial Intelligence kwa sasa.

Artificial Intelligence inaweza kutumika kwenye mawasiliano, uzalishaji viwandani, huduma za afya, usalama, uchambuzi, utabiri, kilimo, biashara, usafirishaji, takwimu na mambo mengine mengi sana.

...

Kutokana na utandawazi na kasi ya ukuaji wa teknolojia kwa sasa Artificial Intelligence si teknolojia ambayo inaweza kuengenezwa na kutumika kwenye nchi zilizoendelea pekee bali hata nchi zinazoendelea zina mambo mengi zinazoweza kufanya na kunufaika kupitia teknolojia hii.

Kumbuka ...

  • AI haihusiani na maroboti pekee.
  • AI si teknolojia ngumu sana au ya bei ghali sana kiasi cha kusema ni mataifa na makampuni makubwa tu ndiyo yanayoweza kuimudu.
  • Kuna mambo mengi kwenye sekta mbalimbali yanayoweza kurahisishwa kwa matumizi ya AI.
  • Kama zilivyo teknolojia zingine AI ina manufaa makubwa na pia ina changamoto zake.